WANAFUNZI 70 katika Shule ya Msingi ya Filbertbay iliyopo Kwamatiasi
wilayani Kibaha, Pwani, wamenusurika kifo baada ya moto mkubwa kuzuka
ghafla katika bweni pamoja na majengo mengine ya shule hiyo.
Tukio hilo lilitokea saa nane usiku wa kuamkia Novemba 11, ambapo
uliteketeza kabisa mabweni ya wanafunzi, chumba cha kulia chakula,
maktaba na miundombinu nyingine ya shule hiyo.
Wanafunzi hao wamenusurika baada ya jitihada za uongozi wa shule hiyo
kufanikiwa kuwanusuru licha ya kutokuwepo gari la zima moto.
Akithibitisha kutokea kwa moto huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani,
Ulrich Matei alisema, moto huo umezuka ghafla katika bweni namba nne la
wasichana.
Matei alisema, moto huo ulianza na kusambaa kwa kasi ambapo pia
uliteketeza bweni lingine la wavulana, madarasa 14 ya kawaida, ofisi
moja, maktaba, ukumbi wa chakula na darasa moja la Compyuta na maeneo
mengine ya mazingira ya shule hiyo.
Taarifa za awali kutoka kwa kamanda huyo zinabainisha kuwa, chanzo cha
moto huo ni hitirafu ya umeme na kwamba uchunguzi unaendelea.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Filbet Bay alikiri moto kuteketeza majengo
hayo na kuongeza kuwa kwa sasa ni mapema mno kueleza thamani halisi ya
madhara yaliyopatikana.
Tukio hilo la Moto limetokea siku mbili tangu tukio jingine kutokea na
kuteketeza maduka katika eneo la Mailimoja mjini Kibaha huku gari la
zimamoto likidaiwa kuwa katika matengenezo na hivyo kutegemea gari
kutoka jijini Dar es Salaam



0 comments:
Post a Comment