Tuesday, 11 November 2014

Maelfu wamzika Amigolas, JK amlilia

MAELFU ya watu walijitokeza jana kumzika aliyekuwa mwanamuziki mahiri wa muziki wa dansi nchini, Khamis Kayumbu maarufu Amigolas katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Walikuwapo wasanii wa muziki, maigizo, wasanii wa zamani, wa sasa pamoja na makundi mbalimbali ya muzi ki. Mwili wa mwanamuziki huyo ambaye hadi mauti yanamkuta alikuwa kiongozi wa bendi ya Ruvu Stars inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), alipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele saa tisa alasiri.

Mwanamuziki huyo aliyewahi pia kutamba na bendi ya Twanga Pepeta akiwa mmoja kati ya waanzilishi wake, alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa.

Alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo alichangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya muziki wa dansi nchini. Alikuwa mahiri zaidi wa kucheza, kuimba, kutawala jukwaa pamoja na kuchombeza vionjo mbalimbali vya muziki.

Wanamuziki mbalimbali walimzungumzia mwanamuziki huyo kwa kusema kuwa alikuwa ni chachu ya maendeleo ya sanaa kwa kuwa alikuwa hana majivuno na alikuwa akiwasaidia wasanii wengi.

Mwanamuziki Robert Hega maarufu kama Katapila, alisema Amigolas alikuwa na maisha mazuri kwa wasanii wenzake hata nje ya kazi yake ya muziki.

Alisema alikuwa akishiriki katika kutoa mawazo ya kuendeleza muziki hata kwa wasanii wasiokuwa kwenye bendi aliyokuwapo.

“Huyu kwangu binafsi nilifanya naye kazi pale Twanga akiwa kama kaka yangu na alikuwa anajua muziki vyema kuliko hata ambavyo ilikuwa ikifahamika, lakini hakuwa na nyodo kabisa,” alisema Katapila.

Mwanamuziki mwingine, Muumini Mwinjuma alisema Amigolas alimshauri mengi na kumtia moyo kuhusu muziki. Moja kati ya nyimbo alizotunga mwanamuziki huyo ni Aminata alioimba akiwa na Twanga Pepeta.

Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha Amigolas.

“Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha mwanamuziki Khamisi Kayumbu kilichotokea tarehe 9 Novemba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake
.
Rais Kikwete alisema anatambua mchango mkubwa wa Amigolas, katika kuhamasisha maendeleo ya nchi kupitia sanaa ya muziki katika kuwafikishia wananchi ujumbe muhimu wa masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Amesema Kayumbu alikuwa mfano unaofaa kuigwa na wasanii wengine kote nchini.

“Kutokana na msiba huu, naomba upokee salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa wanamuziki mahiri hapa nchini, na rambirambi hizi ziwafikie pia wanamuziki wengine kote nchini kwa kumpoteza mwenzao,” alisema.

0 comments:

Post a Comment