Tuesday, 11 November 2014

Asilimia 13 ya Wakazi Mkoani Morogoro hawana vyoo

Ofisa Afya wa Halmashauri ya Manispaa Morogoro, Gabriel Malisa amesema halmashauri hiyo ina kata tano zenye wakazi wasio na vyoo, ambayo ni sawa na asilimia 13 ya wakazi wote wa manispaa hiyo.

Akizungumza ofisini kwake jana, Malisa alisema kuna kampeni maalumu inaendelea ili kukomesha tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha elimu inawafikia wakazi hao ili wajenge vyoo bora.

Alitaja kata hizo kuwa ni Kingorwila, Mzinga, Kauzeni, Bigwa na Mindu. Alisema kuwa mkakati uliopo ni kuhakikisha wakazi hao wanajenga vyoo ili kusaidia kuondokana na magonjwa ya kuambukiza.

Malisa alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa hapa nchini ni asilimia 22 tu za kaya za mijini, ndizo zenye vyoo bora. Alisema kuwa katika maeneo ya vijijini ni asilimia 9 tu ya wakazi walio na vyoo bora.

Alisema Manispaa hiyo itakuwa mwenyeji wa siku ya kunawa mikono na usafi wa mazingira kitaifa kuanzia Novemba 14 na kilele chake ni Novemba 19. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Choo bora na mikono safi kwa afya bora, utu na usawa.”

0 comments:

Post a Comment