WABUNGE wameshutumiana vikali juu ya baadhi yao kutumiwa na kampuni
kubwa za kigeni kukwamisha kupitishwa kwa miswada miwili, inayotarajiwa
kuwasilishwa na Serikali katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea
mjini hapa, yenye lengo la kupunguza au kufuta misamaha ya kodi.
Marekebisho chanya yanayotajwa katika miswada hiyo ni pamoja na yale
yanayowaondolea mawaziri na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), mamlaka
ya kutoa misamaha ya kodi kama ilivyo sasa.
Hata hivyo, wabunge wamesema wataipitisha miswada hiyo baada ya
kufanyiwa marekebisho mbalimbali katika maeneo ambayo bado yanatoa
mianya kwa misamaha ya kodi kutolewa, au fedha za umma kuibwa, kama
ilivyokuwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Hayo yaliibuka jana wakati wabunge hao wakichangia kwenye semina ya
kujadili na kupanua uelewa juu ya miswada hiyo; Muswada wa Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) na Muswada wa Usimamizi wa Kodi (TAA) ya mwaka
2014.
Semina hiyo iliyofunguliwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai jana,
ilihusisha wabunge wa Chama cha Bunge cha Kupambana na Rushwa (APNAC),
chini ya Makamu Mwenyekiti, Habibu Mohamed Mnyaa na Katibu Mkuu wake,
Vita Kawawa na Muungano wa Asasi Tisa zisizo za Kiserikali (NGOs), chini
ya Mwenyekiti wao, Godfrey Wawa.
Shutuma kwa wabunge
Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM) alikuwa wa kwanza kutoa
madai hayo, akisema kuna karatasi zinasambazwa kwa wabunge na watendaji
wa Serikali, zikitoa maelekezo kwao kutetea kutofutiwa misamaha ya kodi
wakati miswada hiyo itakapokuwa ikijadiliwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti (Mnyaa), tuna upungufu mkubwa wa uadilifu
katika nchi hii. Mtu akipewa nafasi basi malengo yake makubwa ni
kujineemesha yeye na familia yake na si Watanzania. “Leo hii tumekuwa na
misamaha ya kodi inayotolewa kwa lengo si la kuwanufaisha Watanzania
bali ya kuneemesha matumbo ya watu. Leo hapa tunajadili umuhimu wa
misamaha hii ya kodi kufutwa lakini waheshimiwa wabunge, hivi vikaratasi
vikaratasi vinavyopita ili tusifanye uamuzi ni lazima tuvikatae,”
alisema Jaffo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) alisema ili kuondoa
misamaha ya kodi na kuongeza makusanyo ya Serikali ni lazima viongozi wa
juu wa Serikali na wabunge, wawe na dhamira ya dhati ya kukabiliana na
kampuni kubwa za kigeni na wahisani.
“Mheshimiwa Mwenyekiti nasema hivyo kwa sababu hawa tunaopanga
kuwaondolea misamaha ya kodi, ndio leo hii wanaotuwekea vikwazo vya
kiuchumi na kukataa kuchangia fedha kwenye bajeti yetu. Wakati umefika
sasa wa kufuta misamaha yote ya kodi tunayowapa ili nao wakae na fedha
zao,” alisema Bulaya.
Alisema pamoja na kuwepo kwa miswada hiyo ili kupata sheria mpya,
lakini sheria zinaweza kuwepo lakini usimamizi wake ukawa mbovu kutokana
na ukosefu wa dhamira ya dhati kwa viongozi kukataa matakwa ya kampuni
hizo kubwa za kigeni.
“Leo hii tunataka kuongeza makusanyo, lakini tumewahi kujiuliza hata
hizi fedha tunazozikusanya zinatumika vipi? Tumeona katika halmashauri
zetu namna ubadhirifu wa fedha zinazoelekezwa huko unavyotokea, lakini
pia kuna rushwa ya ajabu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ambayo ni lazima idhibitiwe haraka,” alisema Bulaya.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keisy alisema anazo taarifa kwa
kampuni kubwa kupanga njama za kutumia wabunge, kukataa miswada hiyo ya
kuziondolea kodi kampuni hizo kupitishwa.
“Hawa wabunge wanaopitishiwa vikaratasi hivyo wanafahamika na wamo
humu humu ndani,” alisema. Alisema hali ya ukwepaji kodi nchini ni ya
kutisha hivi sasa na kwamba zipo kampuni tano za kigeni, zinazoendesha
shughuli zake katika Bandari ya Dar es Salaam bila kulipa kodi na hakuna
chombo cha Serikali, kinachojaribu kuzikagua kampuni hizo.
“Kwa kweli
Mwenyekiti hali ya ukwepaji kodi ni ya kutisha, imefika mahala sasa
tunatoa misamaha ya Sh trilioni 1.8 wakati hawa wahisani
tunaowanyenyekea wanatusaidia kama Sh bilioni 900 tu, yaani kiasi cha
msamaha tunaowapa ni mara mbili ya fedha wanazotuchangia,” alisema
Keisy.
Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Tarime, Chacha Nyangwine (CCM)
alisema ni lazima sasa taifa liachane na utegemezi wa wafadhili katika
kujenga uchumi, badala yake liunganishe nguvu ya wawekezaji wazawa
katika kumiliki njia kuu za uchumi hususani mafuta, gesi na maliasili
kutokana na dalili za wazi za wawekezaji wa nje kuhujumu uchumi wa
Taifa.
Maeneo yanayorekebishwa, upungufu
Awali, Mtaalamu wa Uchumi nchini, Silas Olang alisema katika miswada
hiyo ya Serikali, maeneo yaliyopendekezwa kufutiwa misamaha ya kodi ni
pamoja na ile inayohusu misamaha ya VAT katika kifungu cha 6 (i) (ab).
Kifungu hicho kinalenga wawekezaji wenye hati ya misamaha ya kodi
kutoka TIC, wanaowekeza kwenye maeneo ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji
(EPZ) na SEZ, wale wanaotambuliwa na Mkakati wa Hadhi ya Mwekezaji,
kupunguzwa kwa makundi maalumu yanayopewa misamaha ya kodi na kupunguzwa
kwa mamlaka ya Waziri katika kutoa misamaha hiyo ya kodi.
“Mapendekezo haya ya miswada hii itapunguza sana uwezekano wa kuwepo
kwa matumizi mabaya ya madaraka kunakosababishwa na upendeleo, rushwa na
migongano ya kimaslahi,” alisema Olang.
Kuhusu upungufu wa miswada, alisema ni kutokuwepo kwa vigezo mahususi
vya utolewaji wa misamaha katika huduma za jamii, kama kilimo, afya na
elimu na kushauri vigezo hivyo viwekwe kuleta uwazi na uwajibikaji.
Upungufu mwingine ni kutowekwa kwa ukomo wa kuahirisha kulipa kodi
kutokana na mamlaka aliyonayo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
“Muswada unasema Kamishna Mkuu anaweza kuahirisha kampuni kulipa kodi
lakini haujaweka kikomo, hivyo kampuni inaweza kuahirisha kulipa kodi
miaka na miaka,” alisema.
Alitaja upungufu mwingine kuwa ni kutokuwepo kwa uwazi ambapo alisema
hakuna kifungu kinachoweka masharti ya utoaji taarifa kwa umma juu ya
misamaha na thamani ya misamaha na kwamba kuwepo kwa kifungu hicho
kutaongeza uwazi na uwajibikaji.
Wabunge hao kupitia kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM)
walikubaliana kutoikubali miswada hiyo hadi pale marekebisho
yatakapofanywa kuzuia upotevu wa fedha za umma na pia kuondoa uwezekano
wa fedha kuchotwa kama ilivyotokea kwenye sakata la EPA.
Awali akifungua semina hiyo, Ndugai aliwataka wabunge kuitumia nafasi
hiyo kusoma kwa umakini miswada hiyo na kuiboresha ili kumaliza kilio
cha siku nyingi cha wabunge cha kutaka misamaha ya kodi kupunguzwa au
kufutwa ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.



0 comments:
Post a Comment