Tuesday, 11 November 2014

Azam FC yaleta kocha, ‘nduguye’ akina Kipre

George Nsimbe ‘Best’
George Nsimbe "Best"
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC wameimarisha kikosi chao kabla hata ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa kusajili beki wa kati, Serge Wawa wa Ivory Coast.

Aidha, Azam FC imeleta Kocha Msaidizi mpya, George Nsimbe ‘Best’ na kumtupia virago Ismailla Diarra wa Mali ili kufuata kanuni za ligi zinazotaka klabu kusajili wachezaji watano wa kigeni.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Meneja wa Azam FC, Jemedari Said alisema Wawa aliwasili nchini jana na leo anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusajili.

“Wawa ameshafika leo asubuhi (jana) na kesho (leo) atafanyiwa vipimo vya afya kama yuko safi. Tutamsubiri wakala wake tarehe 12 (kesho) aje tusaini mkataba,” alisema Said akimzungumzia beki huyo ambaye alikuwa akiichezea El Merreikh ya Jamhuri ya Sudan.

“Na pia tumevunja mkataba na Diarra ili kuwa na idadi sawa ya wachezaji wa kigeni.”
Alisema Diarra walisaini naye mkataba wa mwaka mmoja unaotarajiwa kumalizika Juni mwakani, hivyo wameshamalizana naye na kwa sasa mchezaji huyo yupo huru.

Hakucheza mechi hata moja ya Ligi Kuu Bara. Wawa anakuwa mchezaji wa tatu wa Ivory Coast kusajiliwa na Azam FC akitanguliwa na pacha wawili, mshambuliaji nyota Kipre Tchetche na kiungo Kipre Balou.

Kuhusu Kocha Msaidizi Nsimbe ‘Best’, Said alisema wameshamalizana naye na jana jioni alitarajiwa kurudi kwao Kampala kabla ya kuja kuanza kazi baada ya wiki moja.

“Tumemalizana na Best, tumesaini naye mkataba wa miaka miwili leo (jana) na jioni atakwenda kuweka sawa mambo yake ya kifamilia atarudi kuanza kazi rasmi wiki ijayo,” alisema meneja huyo.

Best anachukua nafasi ya Kally Ongala anayedaiwa kuwa na mpango wa kwenda nje ya nchi kuongeza elimu zaidi ya taaluma ya ukocha, ingawa taarifa zinadaiwa ametupiwa virago.

Best atasaidiana na Joseph Omog kuinoa Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Azam FC imefanya mabadiliko baada ya kutetereka na kupoteza mechi mbili kwenye ligi.

Kwa sasa ina pointi 13 sawa na Yanga iliyo kwenye nafasi ya pili. Mtibwa Sugar ndio inaongoza ikiwa na pointi 15.

Ligi Kuu imefika katika raundi ya saba na imesimama kuanzia jana kupisha mechi za kalenda ya Fifa kati ya Taifa Stars dhidi ya Swaziland itakayochezwa Jumapili wiki hii mjini Mbabane na kisha michuano ya Kombe la Uhai na Kombe la Chalenji kwa njia za Afrika Mashariki na Kati ambayo pia iko katika hatihati.

0 comments:

Post a Comment