Saturday, 8 November 2014

JK amtumia salamu za rambirambi Bendera

 RAIS Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kwa vifo vya watu 12 waliokufa papo hapo na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa kutokana na ajali ya barabarani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Rais Kikwete alisema: “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa za vifo vya watu 12 waliopoteza maisha papo hapo na kusababisha simanzi kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki zao, huku taifa likipoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo yake kutokana na ajali za barabarani”.

Rais aliongeza: “Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutokana na ajali hiyo na kupitia kwako, salamu za rambirambi na pole nyingi ziwafikie wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza roho za marehemu wote mahala pema peponi, amina”.

Pia Rais aliwaomba wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo kuwa na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu mgumu kwao wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao.

0 comments:

Post a Comment