![]() |
| Add caption |
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Patrick Phiri amesema kwa sasa hataraji kikosi chake kupata matokeo mengine ya sare baada ya ushindi bao 1-0 walioupata juzi dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Phiri alisema vijana wake walicheza kwa juhudi kubwa na kupata ushindi huo wa kwanza msimu huu na kufufua matumaini yao ya kunyakua taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara linaloshikiliwa na Azam FC.
“Naweza kusema matokeo ya sare kwa sasa ‘bye bye’ kwa sababu ushindi utatuongezea hamasa katika mechi zinazofuata na kutufanya tucheze kwa nguvu na kuweza kupata ushindi,” alisema Phiri.
Mzambia huyo alisema lengo lake ni kuhakikisha Simba inarudi katika kiwango chake kilichozoeleka na kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kwenye nafasi mbili za juu ili iwe moja ya timu ambazo zinawania taji msimu huu.
“Hatupo mbali sana na timu zinazoongoza ligi kwa hiyo Simba bado ni moja ya timu zinazowania ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu kwa sababu ina uwezo wa kufikia pointi ilizonazo Mtibwa kama tutashinda mechi zetu zilizobaki,” alifafanua Phiri.
Akizungumzia mchezo huo wa juzi, alisema ulikuwa mgumu kwa sababu wapinzani wao, Ruvu Shooting ni timu nzuri na iliwapa upinzani mkali hasa katika kipindi cha kwanza na kumfanya aumize kichwa kutafuta mbinu za kupata ushindi.
“Nawapongeza sana mashabiki, viongozi pamoja na wachezaji wangu kwa kuonesha jitihada kubwa na kuhakikisha tunaondoka na pointi zote tatu, lakini mchezo ule hata Ruvu wangeweza kupata ushindi kulingana na upinzani ulivyokuwa uwanjani,” alisema Phiri.
Ushindi huo umeokoa kibarua cha Phiri aliyepewa mechi mbili kubadili matokeo ya sare na pia matokeo hayo yameivusha timu hiyo kutoka nafasi ya 10 iliyokuwa awali hadi ya saba ikiwa na pointi tisa kibindoni.
Tangu kuanza kwa Ligi Kuu, Septemba 20, mwaka huu, Simba imecheza mechi sita na kutoka sare zote, kabla ya ushindi wa juzi, na kuzua sintofahamu kubwa kwa viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki wake.
Inakwenda katika mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa ya kalenda ya Fifa na Kombe la Uhai na Kombe la Chalenji ikiwa na nguvu baada ya ushindi huo wa kwanza msimu huu. Ligi itarejea tena Desemba 26, mwaka huu.




0 comments:
Post a Comment