Wednesday, 12 November 2014

Nagu: Tunatambua mchango wa sekta binafsi

  Nagu: Tunatambua mchango wa sekta binafsi
Dr. Mary Nagu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi, hususan wawekezaji wa ndani na wafanyabiashara katika kukuza uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo nchini. 

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa 15 wa mwaka wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), akisema kuwa shughuli mbalimbali zinazofanywa na sekta binafsi katika sekta zote za uchumi pia zimekuwa zikichangia kukua kwa pato la Taifa.

“Mchango wa TPSF katika ukuaji wa uchumi ni muhimu sana, hivyo serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha mchango wa sekta binafsi unaongezeka ili tuweze kujenga uchumi imara na wa kisasa kama ilivyoelekezwa kwenye dira yetu ya maendeleo ya mwaka 2025,” alisema.

Aidha, Dk. Nagu alisema kukosekana kwa uwekezaji kwenye sekta zinazogusa maisha ya watanzania walio wengi kumesababisha washindwe kufikia azma ya kujenga uchumi imara na kuondoa umaskini.

“Ili kuondokana na jambo hili la baadhi ya watu kushindwa kuwekeza katika sekta zinazogusa maisha ya jamii, ni muhimu kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya watanzania watakaoingia kwenye tabaka la kati katika sekta zote, kusudi tuongeze kiwango cha uwekaji wa akiba na kujenga soko litakalokuwa chachu ya kuongeza shughuli za uzalishaji na uwekezaji,” alisema.

Dk. Nagu pia alitoa wito kwa taasisi zote za serikali kutimiza wajibu wao wa kuhidumia sekta binafsi kwa kasi na viwango vya ubora wa huduma vinavyokubalika kimataifa ili kwa pamoja wafikie malengo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.

Naye Mwenyekiti wa TPSF, Reginald Mengi alisema bila amani na utulivu katika nchi sekta binafsi haitaweza kufanya kazi yake kwa weledi unaotakiwa.

Mengi alisema suala la rushwa limekuwa likiongeza gharama za kufanyabiashara na kuiomba serikali kuchukua hatua madhubuti zitakazowezesha wafanyabiashara kufanya kazi kwa amani.

0 comments:

Post a Comment