MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk Mohammed
Gharib Bilal amesisitiza kwamba ni lazima waumini wa dini ya Kiislamu
wawe katika sura halisi ya dini hiyo kuliko inavyotafsiriwa katika dunia
ya leo na kuhusishwa na ugaidi.
Aliwashauri Waislamu kuwa vikundi vyote kama uamsho, IS, Boko Haramu
na al Shabab ambavyo vinabeba sura kwamba eti vinatetea Uislamu, ni
vyema vipigwe vita kwa nguvu zote na Waislamu wote duniani kwani
vinapotosha taswira na maana halisi ya Uislamu kwa kuwa ni vya hatari na
vinaathiri kila mtu wakiwamo Waislamu wenyewe.
Makamu wa Rais alitoa rai hiyo katika hotuba yake ya ufunguzi wa
Ijitimai ya Kimataifa jana iliyoandaliwa na Taasisi ya Fiysabilillah
Tabligh Markaz katika msikiti mkuu wa Ijumaa ambayo ilishirikisha
waumini wa dini hiyo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kabla ya kutoa hotuba hiyo, alipata fursa ya kuswali swala ya Ijumaa
na mamia ya waumini kwenye Msitiki Mkuu wa Ijumaa uliopo barabara ya
Boma, Manispaa ya Morogoro.
Hivyo, aliwataka wanazuoni na Waislamu wote nchini kuwa wana jukumu
kubwa la kuungana na wenzao duniani kote kuufanya Uislamu uchukue sura
yake halisi.
Pamoja na kusema hayo, Makamu wa Rais aliwashukuru wananchi kwa dua
zao njema walizoliombea Bunge Maalumu la Katiba na hatimaye kupata
Katiba inayopendekezwa na hivyo akawakumbusha kila mmoja atumie muda
wake kuisoma vizuri, kuielewa na kuitathimini katiba hiyo pamoja na
kulinganisha na katiba ya sasa.
Hata hivyo, alisema kupitia taasisi ya Fiysabilillah Tabligh Markaz,
wamedhamiria kujenga Hospitali kubwa ya Rufaa katika Jiji la Dar es
Salaam, na tayari kiwanja kimepatikana eneo la Chamazi na ramani ya
michoro ya jengo hilo inaandaliwa ambapo walimwomba Makamu wa Rais awe
mlezi wa Taasisi hiyo.



0 comments:
Post a Comment