Saturday, 8 November 2014

Mwandosya aeleza Bunge faida za safari za JK


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya juzi alilazimika kuweka mambo sawa juu ya usahihi wa ziara za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi.

Profesa Mark Mwandosya alilazimika kusimama bungeni ili kutuliza upepo, kutokana na hatua ya baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni kupotosha kuhusu ziara hizo za Rais, walipokuwa wakichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/16.

Akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu, baada ya Mizengo Pinda kuwa na kazi nyingine nje ya Bunge, Profesa Mwandosya aliwaambia wabunge kwamba Rais haendi nje kuomba, bali anatengeneza uhusiano imara wa kidiplomasia, hatua inayowafanya wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

“Rais haendi katika mataifa hayo kama omba omba kama mnavyopotosha nyie. Anakwenda kuvutia uwekezaji na fedha zinazotolewa hatupewi bure bali ni mkopo. Hata hili bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Kinyerezi, Dar es Salaam ni mkopo na ni matokeo ya ziara za Rais,” alisema Profesa Mwandosya.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo mwenye ushawishi mkubwa, aliwataka wabunge wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, kuisaidia Serikali katika kuboresha Mpango wa Maendeleo wa Taifa, badala ya kutumia muda mwingi kuukosoa bila kutoa suluhisho.

“Nimegundua wabunge wengi mnasimama na kukosoa bila kuboresha Mpango wenyewe. Hii itawafanya wataalamu wetu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango wanaosubiri michango yenu, kushindwa kupata mambo muhimu ya kuboresha Mpango,” alisema Profesa Mwandosya.

Alisema hakuna sababu ya wabunge wanaoaminiwa na wananchi katika kuboresha maisha yao, kutoka nje ya mada ya Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo na kuanza kujadili mambo ambayo hayana maslahi kwa taifa.

“Tusiruhusu hisia zetu kutuendesha wakati huu ambapo tunajadili suala ambalo linagusa mustakabali wa Taifa na wananchi wetu,” alisema Profesa Mwandosya aliyekuwa akipigiwa makofi na wabunge wa pande zote.
Wabunge wataendelea kujadili Mapendekezo ya Mpango huo wa Maendeleo ya Taifa uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira, Jumatano.

0 comments:

Post a Comment