Wednesday, 12 November 2014

Dk. Slaa amvaa JK kashfa ya ujangili

Dk. Slaa amvaa JK kashfa ya ujangili
Dr. Slaa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amesema kwamba hakuna namna ambavyo Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inaweza kukwepe kuhusishwa na tuhuma za ujangili wa meno na pembe za ndovu, kutokana na hatua yake ya kushindwa kuwachukulia hatua wahusika licha ya kutamba kwamba anawatambua pamoja na vinara wao. 

Kauli ya Dk. Slaa inakuja siku chache baada ya serikali kukanusha tuhuma zilizochapishwa na gazeti la New York Times la Marekeni, likinukuu ripoti ya Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira (EIA) yenye makao yake jijini London-Uingereza, ikidai kwamba China ilinunua maelfu ya kilo za pembe za ndovu na kuzitorosha kwa kutumia ndege ya Rais wao, Xi Jinping wakati alipozuru Tanzania Machi 2013.

Katika habari hiyo, mwandishi Dan Levin anasema kuwa EIA imehusisha rushwa na biashara hiyo haramu nchini Tanzania hususani kwa wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa kutoka Chama tawala Cha Mapinduzi (CCM), kwamba Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, kulikuwa na tembo takribani 142,000 na wakati huu ambapo amebakiza mwaka mmoja kuondoka, idadi hiyo inakadiriwa kupungua na kubakia tembo 55,000.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Kikwete alikabidhiwa orodha ya siri na vyombo vya usalama ikiwataja wahusika wakuu waliyo nyuma na biashara hiyo ya ujangili, wakiwemo wanasiasa mashuhuri na wafanyabiashara waliokaribu na CCM, lakini ni watuhumiwa wachache waliochunguzwa na kuchukuliwa hatua.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, kuhusu tuhuma hizo, Dk. Slaa alisema kuwa ripoti hiyo inaeleza jinsi maofisa wa China walivyotumia fursa ya kidiplomasia ya kutokukaguliwa kwa mizigo yao, kupitisha bidhaa hizo haramu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).

Alisema kuwa utetezi wa serikali uliyotolewa bungeni na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikianao wa Kimataifa, Bernard Membe kwamba tuhuma hizo zinatokana na wivu na husda wa wabaya wa Tanzania ni dhaifu kwa kuwa haikuwahi kukubali hata mara moja juu ya tuhuma mbali mbali zilizoelekezwa kwake hata zile ambazo baadaye ilibainika ni za kweli.

Dk. Slaa alifafanua kuwa utetezi huo unaweza kufananishwa na ule uliotolewa wakati wa tuhuma za ufisadi wa fedha za EPA ambapo viongozi wa serikali ya CCM walisema ni kelele za chura zisizoweza kumzuia ng’ombe kunywa maji na kwamba baada ya wizi huo kudhihirika serikali ikaamua kuwaomba wezi warudishe fedha hizo kisha wasamehewe.

Aliongeza kuwa viongozi wa vyama vya siasa walishawapigia kelele viongozi wa serikali watoe kauli wakati meli inayomilikiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ilipokamatwa na meno ya Tembo nchini Vietnam na kwamba hakukuwa na kauli yoyote.

“Rais hakutoa kauli licha ya kwamba Kinana alikiri meli ni yake ila akasema hamjui aliyesafirisha mzigo huo. Rais alikaa kimya, vyombo vya ulinzi kimya utafikiri meno yale yalisafirishwa pasipo kuwa na vibali wala kupitia katika bandari yetu.

“Rais Kikwete akiwa nchini Uingereza, alisema anayo orodha ya majina 40 ya watu wanaojihusisha na ujangili na kwamba kinara wao yuko jijini Arusha, lakini mpaka leo hawajakamatwa. Ingekuwa kauli hii imetolewa na Dk.Slaa labda wangesema ni maneno yake, lakini Tembo wanaouawa wapo Selou,Serengeti na mbunga zingine nchini, Twiga wanaondoka, michanga ya dhahabu inabebwa ila husikii hatua zimechukuliwa,” alisema Dk. Slaa.

Alihoji kuwa katika hali kama hiyo huwezi kumuondoa Rais katika suala la kuwalinda wanyamapori wetu wasiuawe na majangili na kwamba kama kauli hiyo ingesemwa na watu wengine isingekuwa na tatizo, lakini kwa Rais lazima hatua zingechukuliwa.

“Lakini naawaambieni haya yatakoma pale Watanzania watakapokataa kugeuzwa shamba la bibi kwa kuachana na CCM, maana ndani ya chama hicho kwa misingi ya kifisadi waliyojiwekea hata aje malaika hawezi kukiongoza kwa uadilifu, isipokuwa ataungana nao katika ufisadi,”alisema.

Dk. Slaa alisema ni ajabu kwa Waziri Membe kukanusha kuwa hakukuwa na meno na pembe za ndovu katika mizigo iliyotajwa wakati yeye hakuwa miongoni mwa waliopakia mizigo hiyo, kwamba kiutaratibu mabegi ya kidiplomasia yanafungwa na watumishi wa balozi husika hali inayowafanya hata maafisa usalama wasiweze kujua kilichomo ndani yake kwa kuwa hayakaguliwi.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, Membe ni mtu wa ajabu anayetafuta sehemu ya kukimbilia kwa ajili ya kujificha huku akijua hana ushahidi wa hayo anayoyasema. Alitolea mfano akisema kuwa siku za nyuma aliwahi kusema CHADEMA inafadhiliwa fedha na mataifa ya Magharibi kwa ajili ya kuiangamiza nchi bila kutoa uthibitisho hadi leo.

Alisema kuwa katika mataifa yanayoizunguka Tanzania, mambo haya huwezi kuyasikia kwa sababu viongozi wao wako makini na rasilimali za nchi.

“Tulisikia kule Kenya zilipokamatwa pembe za ndovu, zilichomwa. Tanzania ni mara ngapi tumekamata, mlimsikia aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Balozi Khamis Kagasheki akiongoza ukamataji maeneo ya Msasani lakini mmesikia wapi zimeenda pembe hizo,”alihoji.

0 comments:

Post a Comment