HATIMAYE kilio cha wagonjwa kupoteza maisha na kuteseka, kutokana na
uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali nyingi nchini, kunakotokana na
Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) kuishiwa dawa, kwa kutolipwa zaidi ya Sh
bilioni 102 na Serikali, kimesikika.
Jana wabunge kadhaa walisimama na kuibana Serikali wakitaka sasa
suala hilo litolewe maelezo, huku baadhi wakipinga hatua ya vikao vya
Bunge kuendelea kama fedha hizo hazitalipwa.
Hatua hiyo ilitosha kuifanya Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu ambaye anakaimu pia nafasi ya Kiongozi wa
Shughuli za serikali bungeni, Profesa Mark Mwandosya kuahidi kuwa tamko
la serikali kuhusu hali ya vifaa tiba na dawa nchini litatolewa wiki
hii.
Mbunge wa kwanza kulalamikia hali mbaya ya huduma za matibabu nchini,
alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) ambaye aliomba
Mwongozo wa Spika, na kuelezea namna wanawake wenye saratani ya shingo
ya kizazi wanavyopata mateso, kutokana na kuharibika kwa mtambo maalumu
wa mionzi katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.
Alisema hali hiyo inatokana na mtambo wa pili katika hospitali hiyo
kuwa mbovu kwa muda mrefu sasa bila kutengenezwa, hatua iliyofanya
wagonjwa kutegemea mtambo mmoja uliokuwa umesalia, ambao nao sasa
umeharibika.
Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Khasim Ahmed (CUF) yeye alipinga vikali
hatua ya vikao vya Bunge kuendelea, huku deni la zaidi ya Sh bilioni
102 la MSD likishindwa kulipwa na serikali na kufanya wagonjwa kuendelea
kuteseka.
Mbunge huyo ambaye alitoa hoja na kuungwa mkono na wabunge wengine,
alisema hakuna sababu kwa Bunge hilo kuendelea na hivyo alitoa hoja ya
kuahirishwa kwa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea ili fedha za
wabunge, zikalipe deni la MSD.
Hatua hiyo ilitosha kumfanya Mwandosya kusimama na kutoa ahadi ya
Serikali ya kuwasilishwa kwa tamko maalumu la Serikali bungeni wiki hii
kuhusu hali ya vifaa tiba, ikiwemo pia suala la deni la MSD.
Mbali ya suala la MSD, Waziri Mwandosya akijibu mwongozo wa Mbunge wa
Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) kuhusu wakulima kukosa masoko
na kulemewa na mazao ambayo sasa yanakaribia kuoza, pia alisema Serikali
kupitia kwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza
itawasilisha tamko wiki hii.
Ahadi hiyo ya Waziri Mwandosya ilipokelewa kwa furaha na wabunge
wengi, ambao baadaye wakichangia kwenye muendelezo wa hotuba ya
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2015/2016, waliipongeza
Serikali kwa ahadi ya kushughulikia suala hilo la MSD.
Tangu kuanza kwa Mkutano unaoendelea wa Bunge, suala la deni la MSD
limechukua sehemu kubwa ya mjadala, hatua ambayo bila shaka ndiyo
iliyoifanya Serikali kuamua kulitolea tamko kwa lengo la kueleza
mikakati ya kuokoa maisha ya Watanzania wanaoteseka hospitalini.
Mbunge mwingine ambaye amewahi kupendekeza Bunge kuahirishwa ili
fedha wanazolipwa zikalipe deni la MSD kuiwezesha Bohari hiyo kununua
dawa, ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), aliyetoa hoja hiyo wiki
iliyopita.
Naibu Spika, Job Ndugai mara zote ambazo suala hilo limetajwa
bungeni, amekuwa akisema ni suala zito na kubwa, lakini amekuwa
akiwaomba wabunge kuvuta subira wakati Serikali ikiendelea kulifanyia
kazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu na wa uhakika.