![]() |
| Uharibifu wa mazingira |
Taasisi ya Raslimali za Afrika ya Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa (UNU-INRA) yenye makao makuu nchini Ghana, wiki iliyopita, iliendesha mafunzo maalumu mjini Lusaka, Zambia, yaliyolenga kuelezea hatari kwa viumbe hai duniani.
Lengo la mafunzo lilikuwa ni kuwajengea uwezo watafiti, wafanyabiashara, wanamazingira na wachumi ili watambue mambo ya hatari kwa uhai yanayoweza kujitokeza katika shughuli zao za kila siku na jinsi ya kuyakabili.
Waliendesha mafunzo hayo chini ya kaulimbiu Weka Mazingira Mazuri ya Shughuli za Makundi ya Kijamii ili Kuimarisha na Kuendeleza Mahitaji kwa Uhai.”
Hii ni kaulimbiu ambayo inahamasisha shughuli mbalimbali ili ziendane na mipango ya mapinduzi ya kijani barani Afrika.
Haya ni mapinduzi yanayolenga kuimarisha kilimo kupambana na njaa na wakati huohuo kuhifadhi mazingira kwa lengo la kukabili matatizo yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mchumi na mtafiti wa UNU-INRA, Dk Calvin Atewamba anasema binadamu ana kila sababu ya kujutia kwa kuharibu mazingira wakati akiendesha shughuli mbalimbali ili kupata chakula na kufanya biashara.
Alisisitiza kuwa “shughuli zote za kijamii hapa duniani zina matokeo chanya au hasi kwa mazingira. Kinachotakiwa kifanyike ni jamii kuelimishwa ili kutekeleza malengo ya Afrika katika kufikia mapinduzi ya kijani katika uchumi”.
Alitoa mfano wa shughuli zinazochangia athari za mazingira kama vile uvunaji kupita kiasi wa raslimali za bahari, uchafuzi wa mazingira na kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Dk Atewamba anasema jamii kwa sasa inahitaji kuwekewa mfumo ambao utasimamia na kutathmini shughuli mbalimbali ili kuelekeza nini kifanyike kwa lengo la kupunguza athari za mazingira zinazosababishwa na shughuli za binadamu.
Kufanya hivyo, Dk Atewamba anaamini, kutainua hadhi ya binadamu kwa kuboresha mazingira yanayoendeleza uhai.
Mkurugenzi wa UNU-INRA, Dk Elias Ayuk anaamini kuwa ipo haja ya kuweka kiunganishi kati watafiti wa mazingira na jamii kwa kuwa shughuli za kila siku za binadamu ndizo zinachangia athari za mazingira.
Nchi zilizokuwa na uwakilishi kwenye mafunzo haya ni Ghana, Cameroon, Nigeria, Kenya, Zimbabwe, Misri, Uganda, Malawi, Benin, Swaziland, Tunisia na Zambia




0 comments:
Post a Comment