Jeshi la polisi limetumia maji ya washawasha kutawanya maandamano ya wanawake wa chadema waliokuwa wakiandamana kutokea kinondoni kuelekea ikulu jijini Dar es salaam kwa lengo la kumshinikiza Rais jakaya kikwete kutosaini Rasimu ya tatu ya katiba iliyopendekezwa Bungeni mjini Dodoma hivi karibuni.
ITV ilitia timu katika mtaa wa togo Kinondoni jijini Dar es salaam na kushuhudia baadhi ya wafuasi wa Chadema kutoka Baraza la wanawake wakiwa katika ofisi tayari kujiandaa na maandamano hayo ambapo Mwenyekiti wa Bawacha taifa halima mdee akizungumza na vyombo vya habari akasema maandamano ni haki,na katiba ya jamhuri ya muungano wa tanzania inaruhusu watu kuandamana.
Licha ya askari kuonekana kujipanga katika maeneo hayo ya kinondoni kudhibiti maandamano hayo lakini wanawake hao wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa Bawacha halima mdee walianza Maandamano.
Katika kudhibiti maandamano hayo jeshi la polisi walitumia maji ya washawasha kutawanya wafuasi hao wa Chadema na kujikuta wakikimbilia katika Baadhi ya vibanda vya eneo hilo.
Ghafla ITV ilishuhudia mwenyekiti wa Bawacha taifa Halima Mdee akishikiliwa ndani ya moja ya kibanda alichokimbilia huku katibu wake wa jimbo la kawe naye akitiwa mbaroni.
Baada ya baadhi ya waandamaji hao kushikiliwa,ITV ilizunguka katika maeneo mbalimbali ikiwemo Fire,Mnazi mmoja,Pam Beach,upanga na kukuta maeneo yote hayo yakiwa hayana waandamaji,ambapo katika kituo cha polisi ostebay hali ilikuwa tofauti baada ya watu wakiwemo waandishi wa habari kuzuiliwa kuingia katika kituo hicho huku Magari yanayofika kituoni hapo nayo yakizuiliwa na askari polisi ambapo baada ya kufika baadhi ya wafuasi wa Chadema mzozo ukatokea.
Licha ya ITV kuweka kambi katika kituo hicho kwa zaidi ya saa 7 lakini mpaka inatoka katika eneo hilo bado viongozi wa chadema ngazi ya juu walikuwa hawajaonekana katika kituo hicho licha ya katibu mkuu wa chadema Mh Wilbrod Silaa kuzungumza na ITV kwa njia ya simu na kusema kuwa tayari wanasheria wa chama chao watakuja kushughulikia sakata hilo.



0 comments:
Post a Comment