Sunday, 5 October 2014

Mwigulu afunguka urais 2015


Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba









 Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema ameanza kuchangiwa fedha na Watanzania wanaoishi ughaibuni ili zimsaidie iwapo ataamua kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu bungeni jana, Mwigulu alisema amesikia makundi mbalimbali, wakulima, wafugaji na wanafunzi wa elimu ya juu, walitoa tamko lao juu ya kumtaka kugombea nafasi ya urais.
“Wakulima na wafugaji walisema kuwa nikigombea watachangishana fedha za kampeni kwa kutambua mimi ni mtoto wa maskini na mimi ni maskini,”alisema na kuongeza;
“Wanafunzi wa elimu ya juu walisema kuwa wao watatembea kwa miguu kuhakikisha kuwa kura zinatosha. Kuzungusha fomu niende tu siko pekee yangu.”
Alisema na walimu pia baada ya kupata mishahara kwa wakati sasa wamemwomba kugombea nafasi hiyo ya juu kitaifa.
“Watanzania walioko nje ya nchi walisema wanachangishana na kimsingi wameshaanza kuchangishana ili kuhakikisha kwamba nagombea,” alisema na kuongeza,
“Mimi naendelea kusema ni vizuri watu kukutathmini kwa sababu jambo la urais si kujaza nafasi ni kazi watu wanakutuma uwafanyie na wewe uwajibike kwao na wala si jambo la kutaka tu.”
Alisema wanakutuma kuifanya kazi hiyo baada ya kupima changamoto walizonazo na kuona nani anaweza kufaa katika kuzitatua changamoto hizo.
“Sauti ikiwa kubwa hivyo ni jambo jema ambalo wanaona kuwa unaweza kufanya kazi hiyo vizuri. Naheshimu sana mawazo yao, lakini kwa sasa nataka niweke nguvu katika usimamiaji wa bajeti ya serikali, sera na miradi ya serikali,”alisema na kuongeza:
“Na naweka mkazo kwenye majukumu haya niliyopewa ya sasa. Na mimi huwa ni kawaida yangu jukumu lolote ninalopewa najitahidi kufanya kwa nguvu zote, kwa moyo wote ili Watanzania waweze kunufaika.”
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alisema muda ukifika ataongea kuhusu kama anagombea urais ama la.
“Mimi niko pia katika chama kwa hiyo naheshimu miiko ya chama, taratibu za chama kwa hiyo chama kitakaporuhusu watu waanze harakati hizo ndiyo tutasema,”alisema

0 comments:

Post a Comment