
MWANASHERIA mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Tundu Lissu, amemkingia kifua mgombea urais wa chama hicho, Edward
Lowassa akisema hahusiki na sakata la Richmond.
Lissu ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete
kunukuliwa na gazeti moja akisema kuwa muhusika wa Richmond ni yule
anayetembea na Lissu katika kampeni huku akimtaka amtaje kabla Rais
Kikwete hajafanya hivyo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Shule
ya Msingi ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro jana, Lissu
alimtaja kwa jina kigogo wa serikali akisema ndiye muhusika mkuu wa wa
Richmond na si Lowassa.
Kauli hiyo ya Lissu haitofautiani na ile ya Lowassa aliyoitoa
alipokuwa akijiunga na Chadema ambapo alisema katika moja ya vikao vya
serikali vya kujadili sakata hilo, kiongozi mmoja alisema amepata amri
kutoka ngazi za juu kwamba asaini mkataba wa kampuni hiyo.
Lissu alisema ni vema Watanzania kutambua kuwa mmiliki halali wa
Richmond ambayo imebadilishwa majina kutoka Dowans hadi Symbion kwa sasa
yupo ngazi za juu serikalini.
‘’Huyu mzee wa watu wameshampaka matope vya kutosha na wala hajatoka mbele za watu kulalamika, anatumia busara zaidi.
‘’Tunaishangaa serikali kuendelea kuwadanganya wananchi bila ya
huruma kwa kudai kampuni hizo zote zinamilikiwa na Lowassa, kama
kungekuwa na ukweli wowote, kwanini wanaendelea kulipa hayo madeni ya
mabilioni ya fedha?
“Ni lazima Watanzania watambue kuwa Richmond ilijadiliwa bungeni
ikiwa chini ya mwenyekiti wake Dk. Harisson Mwakyembe ambaye alikuwa
kwenye kamati ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Kampuni ya Richmond na
mwishowe kuja kuibuka kashfa ya mafisadi ambao walikuwa 11,” alisema na
kuongeza.
“Katika mlolongo wa mafisadi waliotajwa namba tisa alitajwa Lowassa
wakati akiwa waziri mkuu, lakini hakuhusika moja moja na suala hilo,”
alisema.
Lissu alisema katika orodha hiyo namba 10 alitajwa kiongozi mmoja
mstaafu na baadae akataja tena jina la kigogo mwingine ambaye alisema
huyo ndiye mmiliki wa kampuni hiyo.
Alisema Lowassa ambaye anatembea naye katika kampeni zake hahusiki
hata kidogo na suala hilo ila aliwajibika kisiasa ili kuiokoa serikali,
kwa kuwa alikuwa msimamizi wa serikali hiyo.
Lissu alisema ili kuondoa mfumo mbovu ni lazima wahakikishe
wanaing’oa serikali iliyopo madarakani kwa kipindi cha muda mrefu, kwani
hiyo ndio chanzo kikuu cha umaskini.
Lowassa: na wakulima
Kwa upande wake Lowassa, alisema serikali yake itakuwa rafiki kwa
wakulima na wafugaji na kuwa atatoa elimu bora bila malipo yoyote.
“Hakutakuwa na mambo ya michango ya ajabu ajabu, tutatoa elimu ya bure lakini iliyo bora,” alisema.
Kuhusu suala la viwanda vya miwa, alisema atahakikisha viwanda vinavyowezekana vitarudishwa mikononi mwa serikali.
Alisema pia kuwa, wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwamo mama lishe na bodaboda, atawahakikisha wanaendelea kuwa rafiki zake.
Sumaye: CCM inahukumiwa kwa uongo wake
Waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alisema kwa sasa CCM
inahukumiwa kwa kusema uongo kwa kipindi cha miaka 50 tangu
taifa lipate uhuru
Alisema katika kipindi hicho, chama hicho kimeshindwa kukidhi
mahitaji muhimu ya Watanzania, hivyo wananchi wamechoka kudanganywa .
Aidha Sumaye alidai Watanzania bado wamekuwa wakiishi katika
mazingira magumu na yenye shida pamoja na CCM kuja na sera
yake ya uongo ya maisha bora kwa kila Mtanzania .
“Ni wazi hakuna ubishi kama Watanzania sasa wamechoshwa na
uongo wa CCM, ndio maana wametuunga mkono kwa asilimia 100 katika
mikutano yote ya Ukawa pasipo kuletwa na magari kama ilivyo
katika mikutano yao”alisema Sumaye .
Alisema uongo wa CCM unajionesha wazi wazi kwenye sekta ya
kilimo, afya , miundombinu, elimu na kudai kuwa hayo ni maeneo
ambayo yanawatesa kwa kiasi kikubwa na kuyaona maisha kuwa magumu.
Alisema kuwa dalili za Watanzania kuunga mkono ukawa ni
dalili tosha kuonesha wanahitaji mabadiliko ndani ya taifa ,
pasipo kushawishika na pesa .
“Hapa mmekuja kwa upendo wenu na taifa lenu hamjaletwa kwa
magari kama ilivyo katika mikutano yao (CCM),” aliongeza Sumaye .
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda ya Kati wa Chadema,
Mathew Likwina akizungumza na wanachama wa chama hicho alisema
kuwa lengo la UKAWA ni kufanya mabadiliko ya kimfumo.
Alisema kuwa kuondoa mfumo sio kubadilisha kiongozi mmoja wa
ccm , bali ni kuondoa uongozi wote wa CCM usio na mfumo mzuri
katika kuleta maendeleo ya taifa na watu wake .
Aidha alidai kuwa kama Watanzania wataiondoa CCM taifa
linauhakika mkubwa wa kuwa na mfumo mzuri Wenye kujali maslahi
ya wananchi badala ya sasa CCM imekuwa na mifumo ya kujali watu
wachache na familia zao .



0 comments:
Post a Comment