Thursday, 22 January 2015

Mazungumzo ya kutafuta amani Sudan kusini yafanyika mkoani Arusha


Rais Jakaya Kikwete  wa pili kutoka kulia akiwa kwenye mazungumzo ya kutafuta Aman
Mazungumzo ya kutafuta amani SUDAN KUSINI yanaendelea mkoani ARUSHA.
 Habari za hivi karibuni kutoka Arusha zinasema mazungumzo hayo ambayo yanafanyika kwa faragha  
yanahudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais JAKAYA KIKWETE, Rais UHURU KENYATTA wa KENYA, YOWERI MUSEVENI wa UGANDA na SALVA KIIR wa SUDAN KUSINI.
Hatua inayosubiriwa katika mazungumzo hayo ni kutiwa saini kwa makubalino ya amani kumaliza mgogoro baina ya vikundi vinavyopingana ndani ya chama tawala nchini SUDAN KUSINI cha SPLM.

Mazungumzo ya upatanishi kati ya vikundi hivyo yamekuwa yakifanyika chini ya uratibu wa Chama Cha Mapinduzi - CCM yakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu JOHN MALECELA tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

SUDAN KUSINI ilipata uhuru wake kutoka SUDAN mwaka 2011 ambapo hata hivyo mwishoni mwa mwaka 2013 iliingia katika mgogoro kufuatia jaribio la kuipindua serikali ya Rais SALVA KIIR.

Mwezi Novemba mwaka jana kundi la usuluhishi linaloundwa na nchi za KENYA, UGANDA, SUDANI pamoja na ETHIOPIA walisaini makubaliano ya suluhu lakini bado mapigano yaliendelea katika nchi ya SUDAN KUSINI.

Viongozi wengine wanaohudhuria mazungumzo hayo ni pamoja na Makamu wa Rais Dkt MOHAMED GHARIB BILAL, Makamu wa Rais wa AFRIKA KUSINI CYRIL RAMAPHOSA na Dk RIEK MACHAR aliyekuwa Makamu wa Rais wa SUDAN KUSINI.

0 comments:

Post a Comment